Misa takatifu

MISA TAKATIFU,
“JESUS OUR NEW ADAM! THE HIGHEST PRIEST, WE WANT TO MEET YOU”
“GRANT TO US THAT WE MAY COME TO YOU THROUGH MARY THE NEW EVE”

MKRISTU WA LEO ZIJUE, ZIELEWE NA ZIHESHIMU ISHARA MBALI MBALI ZA KANISA KATOLIKI
“ Lakini, ili kufikia lengo hilo kamili, sharti waamini washiriki Liturujia takatifu kwa maelekeo ya moyo mnyofu, walinganishe akili zao na sauti, wafanye kazi pamoja na neema ya Mungu ili wasiipokee bure. Kwa hiyo wachungaji watukufu wanapaswa kuangalia kuwa katika tendo la Liturujia zishikwe sheria zifanyazo maadhimisho yawe thabiti na halali. Wachungaji pia lazima wahakikishe kuwa waamini wanaelewa kinachofanyika na wanashiriki kikamilifu na kufaidi matunda ya maadhimisho hayo”. Rejea Mtaguso wa pili wa vatikano konstitusio juu ya liturjia (sacrosanctum concilium-11).

ZINGATIA: Maelezo na mang’amuzi ya makala hii yasikufunge kutafakari nje ya hapa, kwa yale ambayo unaweza kutafakari na kutanua maana tafadhali fanya, ila kwa yasiyowezekana usijisumbue, Mungu atuongoze kwa Roho wake.
Wakatoliki wa leo tunakosa imani na kuburuzwa na ishara nyingi zitumiwazo na Kanisa letu.Wengi tumekuwa tukizifuata na kuzitumia pasipo kujua maana yake na pengine kuzionea aibu mbele ya kadamnasi. Lakini ukweli ni kwamba ishara hizi tukizielewa na kuzitumia ipaswavyo, zitatutakasa na kutuokoa. Ishara zina hamasa bwana hebu imba wimbo, KWA ISHARA YA MSALABA uone!
Mfano:

IHS ni kifupisho cha neno hili Iesus Hominum Salvator (I.H.S)- likimaanisha Yesu mkombozi wa wanadamu, Alama hii hutumika sana na makasisi wa Kanisa Katoliki Wayesuiti (JESUITS-society of Jesus) lililoanzishwa na Mt. Inyasi wa Loyola Hispania. Andiko hili linaonekana mara Kwa mara kwenye mavazi ya Kanisa Kama vile kasula, stola Na Alba, katika vitambaa vya Kanisa Kama vile vya kutandikia altare Na meza (credensia) na zaidi kwenye hostia hasa zile kubwa.

I.N.R.I ni andiko moja lililojengwa kwa herufi za mwanzo za maneno aliyoandika Pilato kama mashtaka ya Yesu na kwa amri yake kukomelewa msalabani kichwani pa Yesu Yoh 19:19, Iesus Nazarenus Rex Iudaeorum-INRI- Likimaanisha Huyu ndiye Yesu Mnazareti Mfalme wa Wayahudi, kumbe asikudanganye mtu na kusema kuwa alama za Kanisa zina maana mbaya, akisema hivyo mwambie aache tafsiri za Sebuleni(za kizushi) atafute tafsiri za Chumbani(za kweli), uliza mapadre, watawa na walei wenzako wanaojua alama hizo.

MAVAZI YA MASHEMASI, MAPADRE NA MAASKOFU KATIKA IBADA NA MAADHIMISHO YA SAKRAMENTI
Nguo za mashemasi, mapadre na maaskofu zina maana yake na hata vitu vingine visivyo nguo. Kwa kawaida nguo au vitu hivyo vinapovaliwa sala husaliwa., Laiti sala hizo zingelikuwa maarufu kwa waamini wote, maana ya vitu hivyo ingelikuwa wazi kwa wote., wengi husema makasisi mbona wanavaa mavazi mengi na mazuri hivo wakati wa Misa?, huu ni ujinga wa kutojua na kuuliza tu, ukiuliza na kutafuta kwa bidii mambo hayo usingelichonga domo hivo na kujichumia dhambi bure, kimsingi mapadre
hawajataka wao kujivisha mavazi hayo je ulitaka wavae suti, kadeki, bukta, mabuti au jezi za mpira au overall na wakaaadhimishe misa?, la hasha wanatakiwa kuvaa mavazi ya kilturjia!
Mavazi yatumikayo na Padre ni matakatifu kwa sababu yanatumika katika shughuli takatifu na pia yanaamsha uzuri, tafakari na hadhi ya Padre na Mazingira(altare n.k), Kutoka 28:2-,
Wapo watu hasa masista wanaofuma mavazi haya safi mabarikiwa kwa kutumia kipaji chao kwa Kanisa , hata kale ilikuwa hivyo rejea Kutoka 28:3, Msishangae Mitra, bakulum(fimbo ya Askofu) n.k hata enzi za zamani vilikuwepo kwa ridhaa ya Mungu, mfano Haruni kwa kuwa kuhani aliwekwa wakfu akapewa Kofia “mitra” Kut 28:36 na anatajwa ni Mtakatifu “Muamini” wa Bwana,Pia Usishangae makanisa yanavyong’aa kwa shaba hasa ya Kanisa Katoliki na ukaanza kulaani, eti Kanisa linafuja Pesa kwa kulipamba Kanisa, Mungu aliruhusu tuipambe nyumba yake, Kut 30:17-
Tuache kumbania Mungu ndugu zangu, na kama mabinti wa Sayuni walitandaza mavazi na madela yao njiani ili Kristo mfalme apite Mk 11:8, Je sisi hatuna budi kupamba mahali ambapo Yesu anaongea nasi?, je,tuache kupamba tabernakulo nyumba ya Kristo wa Ekaristi kwa dhahabu ?, mbona sisi tunapenda kutokelezea?, na kama padre ni tunu na chombo kitumikacho na Kristo kutolea sadaka ya upatanisho je, tusimvishe kanzu nzuri, alba nzuri, stola nzuri na safi kabisa? Tutakuwa tunachekesha!
Sasa hebu tuyachambue na kuyajua mavazi baadhi katika liturjia yetu! , nakiri kuwa maelezo haya yanatoka katika kitabu aliochoandika Padre Titus Amigu Gombera wa Seminary Kuu ya Mt.Agustino-Peramiho na mtaalamu wa maandiko matakatifu(Teolijia), tutaomba atuwie radhi watoto sisi watundu wa kukopi!,
Amikto: Shemasi, padre au Askofu huko anakojiandaa kwa misa huvaa kitambaa fulani mabegani. Anapoanza kuvaa hugusisha kwanza kichwa huku akisali. Sala hiyo hueleza kitambaa hicho kina maana gani. Kifupi, kitambaa hicho ni mfano wa chapeo anayovaa mwanajeshi wakati wa vita kwa kusudi la kumkinga na mashambulio ya adui. Basi amikto huvaliwa ili kumkumbusha padre au Askofu kwamba analo jukumu la kushindana na shetani, aliye adui mkubwa wa kila binadamu
Alba au kanzu nyeupe: Kwisha kuvaa amikto, shemasi, padre au Askofu huvaa kanzu nyeupe (kwa Kilatini alba maana yake nyeupe). Kanzu hiyo hushauriwa kufikia visigino vya miguu, ndiyo alama kabambe ya ukuhani na siyo kibiriti ngoma fulani.Basi jinsi vazi hilo lilivyo jeupe na safi, shemasi, padre au Askofu hukumbushwa aitunze roho yake kwenye usafi na weupe wake ulingane na vazi hilo. Kwa maana hii kanzu nyeupe zilizopoteza rangi yake kwa ukale au uchafu au kuliwa na mende hazifai. Ndiyo maana ni bora kabisa waamini wakisaidiana na mashemasi, mapadre na maaskofu kusaidiana kupata kanzu safi wakati wote.
Mshipi: Kishapo kiunoni shemasi, padre au Askofu hujifunga mshipi. Mshipi huo una maana ya mfano wa kamba ambazo kwazo Yesu Kristo alifungwa kwenye nguzo kwa ajili ya kupigwa mijeledi. Hivi hukusudiwa kumkumbusha kwamba yeye anasimama mahali pa Yesu aliyekubali kusulibiwa kwa ajili ya watu. Aidha maana nyingine ya mshipi ni kumkumbusha shemasi, padre au Askofu kuishi maisha yake ya kujikatalia ndoa, ndiyo useja. Watawa wa kifranskani hufunga vifundo vitatu kwenye mishipi yao wakiashiria ahadi zao tatu kwa Mungu: useja au ubikira, ufukara na utii.
Stola: Baada ya kuvaa hayo yanayovaliwa, mapadre na maaskofu huvaa stola. Shemasi huivaa kwenye bega la kushoto na kuining’iniza kwa kupandanishwa chini ya kwapa ya kulia. Mapadre na maaskofu huvaa mabegani na kupindiwa kwa mbele ya kifua na tumbo. Stola huvaliwa kwa mfano wa mzigo wa msalaba aliouchukua Yesu mabegani mwake na kuelekea nao Golgotha. Waidha kwao stola ni mfano wa kazi na huduma za mapadre na maaskofu, kazi zinazoweza kuwaangusha kama msalaba
ulivyomwangusha Yesu chini mara kadhaa. Kwa hali hiyo, stola huvaliwa kuwakumbusha mashemasi, mapadre na maaskofu unyeti wa kazi zao zinazoweza kuwadondosha chini wakati wo wote wa maisha yao ya kuelekea mbinguni.
Kasula: Kasula ni vazi pana ambalo mapadre na maaskofu hulivaa juu ya mavazi mengineyo yote. Kwa kawaida kasula huwa imepambwa kwa nakshi na katikati huchorwa au hushonewa msalaba. Msalaba huo hukusudiwa kumkumbusha padre au Askofu Yesu msulibiwa na utumishi wake mwenyewe, yaani kumfuata Bwana wetu Yesu Kristo aliyesulibiwa kwa ajili ya wanadamu wote. Kifupi kasula pia ni mfano wa upendo. Msalaba wa Yesu unawaongoza wanadamu kufahamu ya kuwa upendo wa kweli unatoka msalabani kwa Yesu Kristo aliyesulibiwa. Tunapaswa tulielewe hilo kwa sababu Yesu Kristo mwenyewe alisema, “Hakuna aliye na upendo mkuu kuliko yule atoaye maisha yake kwa ajili ya rafiki zake”.
Bereti: Hii ni kofia ndogo kwa ajili ya wenye daraja takatifu. Kihistoria bereri ilitokana na hitaji la kujikinga na baridi wakati wa kuimba kwaya au maandamano. Ilianza kutumika tangu karne ya kumi. Kwa kawaida ina umbo la pande nne na vilele vitatu. Kwa maaskofu, makardinali na Baba Mtakatifu wana bereti zilizorahisishwa sana hali kuwa vibandiko vidogo tu.
Mintarafu rangi, Baba Mtakatifu hutumia rangi nyeupe kama alama ya kulinda mambo matakatifu ya Kanisa. makardinali nyekundu ya damu alama ya ufia dini, maaskofu nyekundu ya moto alama ya ndimi za moto (kama kushukiwa ndimi za moto katika siku ya Pentekoste) na nyeusi kwa makleri wote. Rangi zinazotumiwa na maaskofu hutawala mavazi mengine, mshipi, vifungo vya kanzu na hata soksi.
Baada ya mavazi wanayoshirikiana wakleri wote katika Kanisa, kuna vitu au mavazi ya maaskofu peke yao. Basi uniwie radhi nilipanue jibu langu hadi huko, yaani niendelee na vitu hivyo pia. Sababu yangu ni moja tu, yafaa tuambizane mambo wazi wazi kusudi niondoe kutoelewana.
Mitra: Neno hili ni la Kigiriki. Ni kofia ya kiliturujia iliyo alama ya haki na hadhi ya kiaskofu. Lakini kama upendeleo wa pekee hutolewa pia kwa viongozi wengine kama vile maabate na viongozo maalumu katika Jimbo. Mitra ni kofia yenye pande mbili zilizochongoka moja ikiwa mbele ya kichwa na ya pili nyuma. Sehemu ya kati inayotenganisha pande hizo mbili huweza pia kukunjika. Kwa upande wa nyuma kuna malepe mawili. Matumizi ya mitra kihistoria yalianza kwenye karne ya kumi na moja ambapo Baba
Mtakatifu Leo XI (1049 – 1054) alimpa mitra Askofu Mkuu Everardo wa Treviri ambaye alimsindikiza Roma. Katika nusu ya pili ya karne ya kumi na mbili maaskofu wengi walikuwa tayari wakitumia mitra mara kwa mara. Maana ya mitra na pande zake mbili zilizochongoka ni alama kwake kwamba kikazi Askofu anayaunganisha maagano mawili: Agano la Kale na Jipya.
Pete: Pete inayovaliwa na wanandoa maana yake ni alama ya uaminfu na mapendo. Ndiyo kisa huvishwa kidole cha pete, kidole ambacho watu wa kale, hasa Warumi walidhani kwamba kina mshipa unaoungana na moyo. Hivi mtu anayevaa pete ya mapenzi kwenye kidole kinginecho amepitwa na dhana ya asili ya pete. Kati ya viongozi wa dini pete ina maana pana zaidi. Yaani pamoja na kwamba pete ni alama ya muungano na uaminifu kadiri ya dhana ya sakramenti ya ndoa, kwa Askofu, Kardinali na Baba Mtakatifu
ni alama ya mamlaka na hadhi. Hivi kuibusu pete ya Askofu, Kardinali au Baba Mtakatifu ni ishara ya kuyakubali mamlaka yake. Kihistoria pete zilianza kama muhuri wa kumbukumbu za ofisi za kiaskofu na halafu zikawa kabisa alama ya kiaskofu. Wanapowekwa wakfu maaskofu hupewa pete kwanza hata kabla ya fimbo ya kiaskofu. Kwa watawa wa kike pete ni alama ya muungano ama ndoa yao na Kristo Yesu.
Lk 5:10b
Fimbo: Fimbo si vazi ila kitu maalumu kwa ajili ya Askofu. Fimbo hutumika kwenye liturujia kuonesha mamlaka ya kiutawala kwa kundi la kondoo yaani wanajimbo. Askofu awapo katika kundi lake ama katika kundi alilopewa ruhusa kulihudumia huielekeza ile sehemu iliyopinda kwa waamini. Kama kundi si lake na si yeye mwadhimisha liturujia rasmi, sehemu iliyopinda ya fimbo yake hujielekezea mwenyewe.
Pallium: Pallium ni utepe mpana kidogo ulio na misalaba myeusi ambao huzungushwa shingoni kama pete. Utepe huu hupewa maaskofu wakuu ama viongozi wa kanda za Kanisa, baada ya kuomba wenyewe, kama alama ya muungano wao na Kanisa la Roma. Basi pallium huvaliwa na Baba Mtakatifu na maaskofu wakuu au hao viongozi wa kanda za Kanisa tu. Hivi kila vazi la padre au Askofu lina maana yake. Nayo yanaweza kutusaidia tuwe na mawazo matakatifu inapotolewa sadaka ya misa takatifu.
Rangi za mavazi ya mashemasi, mapadre na maaskofu katika ibada na maadhimisho ya sakramenti
Sasa nihamie kweny rangi za mavazi. Rangi maarufu ni nne: nyeupe, nyekundu, kijani, urujuani au zambarau na nyeusi.
Nyeupe: Rangi nyeupe ni mfano wa mwangazo na pia wa furaha na shangwe. Kwa sababu hiyo padri anavaa mavazi meupe kwenye Sikukuu za Bwana wetu Yesu Kristo (Kuzaliwa Bwana na kipindi chote
cha Noeli hadi Kutolewa Bwana hekaluni na Tokeo la Bwana, Pasaka na kipindi chote cha Paska hadi Kupaa Bwana Mbinguni na Pentekoste, Ekaristi Takatifu n.k.). Kadhalika rangi nyeupe ni mfano wa utakatifu na usafi wa moyo. Kwa sababu hiyo hutumika vile vile kwenye Sikukuu za Bikira Maria (Kukingiwa dhambi ya asili, Kupalizwa mbinguni, Kuzaliwa Bikira Maria n.k.) pamoja na sikukuu au kumbukumbu za watakatifu wasio wafia dini.
Nyekundu: Rangi nyekundu ni mfano wa damu na moto. Kwa sababu hiyo hutumiwa katika Sikukuu ya Pentekoste pale Roho Mtakatifu alipowashukia mitume kwa ndimi za moto za kuwasha ndani yao moto wa upendo. Hutumiwa vile vile siku zile zinazofanyika kama sherehe, sikukuu na kumbukumbu za wafia dini waliomwaga damu yao kama Yesu Kristo alivyofanya kwa ajili yae binadamu wote.
Kijani: Kila mtu anayo picha ya namna mambo yanavyokuwa wakati wa masika. Yaani baada ya mvua za kwanza mimea, nyasi na mti, huchipua. Hio hutokea muda mfupi tu. Ardhi huwa kama iliyotandikwa zulia zuri la majani. Hapo kila mtu huwa na matumaini ya mavuno mazuri. Basi kwa mstari huu, wote tunaitazama rangi ya kijani kama rangi ya matumaini. Hivyo siku zote tunazozitumia kumtumikia Mungu ni sawa na siku za kutumaini kwamba siku moja, mwishoni mwa maisha haya ya kidunia, tutajaliwa mavuno mazuri, ndiyo uzima wa milele. Kwa sababu hiyo mavazi ya rangi ya kijani hutumiwa wakati wa kipindi kinachoitwa cha mwaka wa Kanisa. Kipindi hicho ni cha majuma thelathini na manne. Yaani ni tangu Jumapili ya kwanza baada ya Tokeo la Bwana hata Jumapili ya mwisho baada ya Tokeo la Bwana na wakati wote kuanzia baada ya Pentekoste. Mavazi hayo, hasa kasula za kijani, hutumiwa katika siku zote za kawaida na kumbumbuku zisizo za pekee.
Urujuani: Rangi hii hujulikana pia kama rangi ya zambarau. Ni rangi ya toba. Kwa sababu hiyo hutumiwa katika kipindi chote cha Majilio, Kwaresima na sikukuu au maadhimisho yote yanayohusika na toba. Ndiyo kisa pia mapadre hutumia stola za urujuani kwenye kiti cha Kitubio.
Nyeusi: Rangi hii ni mfano wa matanga. Kwa sababu hiyo ilitumika sana siku ya Ijumaa Kuu Wakristo wanapokumbuka kifo cha Bwana wetu Yesu Kristo. Pia hapo zamani ilitumika katika misa za mazishi na zile za kuwakumbuka wafu. Siku hizi rangi hii inaachwa kando kwa sababu inaonekana kama kuidhalilisha rangi ya Waafrika. Ikiwa weusi ni alama ya matanga, ina maana wao wanahuzunika siku zote? La, si hivyo. Ndipo basi kwa matanga siku hizi wengi wanatumia rangi ya urujuani na hata nyeupe kwa maana ya kujipeleka walau kiteolojia kwenye furaha ya Pasaka.
Tutavaaje sisi?
Hivi basi ndugu zanguni,tuelewe kwamba mtu huvaa chochote anachoamua kukivaa kutokana na maana ya kitu chenyewe hata kama ikiwa sababu yenyewe ni ya kujipamba tu lakini iwe ni kwa sifa mna heshima ya kumpendeza Mungu(1Petro 3:1-7). Kwa maana hiyo mavazi na vitu wanavyovaa mashemasi, mapadre, maaskofu sawia na watawa vyote vina maana yake na ni kutokana na maana hizo wahusika huvivaa hata kama vitu vingine havionekani kwa nje. Nasi kama waamini tunaomcha Mungu tujitahidi mitindo mbalimbali ya mavazi inayobuniwa na wafanya biashara na wenye viwanda vya mavazi isitufanye kuwa wenda wazimu kupindukia kwa kufuata na kutumia kila mtindo unaoibuka tukijidhania imeandaliwa kwa matumizi sahihi kwetu.Si kweli, maana tukifanya hivyo tunazidi kuwafaidisha wafanya biashara na wenye viwanda vya mavazi huku tukizidi kukiuka mapenzi ya Mungu..(1 Tim.6:10)>Fedha ni chanzo cha maangamizi makubwa ya kila namna kwa mwanadamu anayeiabudu na (K/Torati 22:5 ). Hivyo basi jamii tubadilike kwa kutumia mavazi yenye maana takatifu kwa jamii nzima na siyo kuvaa tu bora liende.
MISA HUFANYIKA WAPI?, Kanisa linashauri Misa takatifu ifanyike mahali pa utulivu na pa kutosha waamini, ndiomaana makanisa mazuri na imara hujengwa, wayahudi walitumia mahekalu na masinagogi kwa ibada yao, leo tuna majengo kwa ajili ya kuadhimisha misa takatifu na ibada mbalimbali, Kristo anasema tutamwabudu katika roho na kweli na siyo katika mlima Fulani tu, kumbe kama hakuna Jengo mahali pazuri hata chini ya mti Misa inafanyika, Kristo alifanya sala milimani na hekaluni hivyo penye uiwezekano tujenge makanisa mazuri kabisa kwa ubunifu mzuri na hiyo ni sanaa nzuri kupita zote kwa maana inahusisha matakatifu, kama hapana uwezekano tusisite kakaa juu ya nyasi na tukamtukuza Mungu, lakini ni kweli hatuwezi kujenga? La hasha! , Kristo alijitahidi kutafuta maeneo tulivu mfano milimani, ufukweni sisi tutashindwaje?, je tunaishi maweni au kwenye “mabangaloo” basi tujenge Makanisa ndugu zangu!, Katika kanisa kama jengo kuna Altare, Tabernakulo, sakristia(sehemu ya kuhifadhia mavazi na yombo vya ibada pia sehemu ya kujiandalia kuhani), kathedrali au kiti cha padre, sanamu takatifu, Msalaba, Mishumaa, Kijumba cha Mtoto Yesu, Kisima cha ubatizo, Viriba vya maji ya Baraka mlangoni, n.k Swala la Kupamba Mama Kanisa ameridhia nanukuu kutoka konstitusio juu ya liturjia “ Kwa bidii ya pekee Kanisa amejitahidi ili vifaa vitakatifu vitumike kadiri ya heshima na uzuri wa ibada; na pia amekubali mabadiliko yale ya malighafi, ya maumbo na ya madoido yaliyoingizwa na maendeleo ya mbinu za sanaa katika mwenendo wa karne” SC-122,
BAADHI YA VIFAA VYA MISA
 Tabernakulo- Ni sehemu ambapo Kristo/Hostia hukaa, huwa ni kama kisanduku kirichonakshiwa na kutengenezwa kwa uimara, hufungwa wakati wote isipokuwa wakati wa
ibada, taa inayowaka daima huwa pembeni yake ikiashiria Kristo yupo na Yeye ni Mwanga.tukitafakari zaidi tunaona Tabernakulo ni Sanduku la Agano jipya(mfano wa Tumbo la Maria Bikira) ambamo Amri mpya ya Upendo(Kristo) inabebwa.
 Siborium- ni kikombe maalumu kwa kuhifadhia hostia takatifu na kugawia kwa waamini, Hostia zinazobaki huwekwa humo na kuhifadhiwa katiak tabernakulo.
 Kalisi- Ni kikombe cha namna yake kitumikacho kuwekea Divai wakati wa Misa. Huwekwa juu ya korporale , Kalisi hufunikwa na Pala.
 Patena- Hiki ni kama kisahani king’aacho kama dhahabu ambacho hutumika kuwekea Hostia kubwa inayotumika katiaka mageuzo wakati wa Misa, Patena huwekwa juu ya Korporale
 Korporale- ni kitambaa kidogo chenye umbo la Mraba cheupe ambacho hutandikwa katikati ya altare juu ya vitambaa vingine vikubwa vya altare, katika kitambaa hiki Mwili wa Kristo katika patena na Damu nya Kristo katika Kalisi huwekwa juu yakwe.
 Purifikatorio- ni kitambaa maalumu ambacho hutumika kusafishia na kukausha kalisi na vyombo vingine wakati wa Misa.
 Monistrensi- ni kifaa maalumu ambamo mwili wa Kristo(Hostia kubwa) huwekwa wakati wa maandamano ya kiekaristi na wakati wa kuabudu siku za alhamisi na nyinginezo inapobidi, ina umbo zuri kama la jua litoalo miale Fulani, monstrance inarangi ya dahabu, mimi naiona kama Ua la matumaini, ua la upendo ambamo BWANA Mkubwa yumo.
 Pala- ni kitambaa kizito na kigumu cha umbo mraba ambacho hufunika Kalisi ili kuilinda divai/damu ya Kristo isichafuke kwa vumbi , wadudu, n.k.
 Mimbari- ni sehemu maalumu ambapo hutengenezwa kwa simenti au ni mbao, Hapo neno husomwa, Homilia hutolewa na matangazo hutolewa.
 Mishumaa- Mishumaa altareni huwakilisha Furaha tuliyonayo Kwa Kristo Yesu.
 Mkate – Ni zao la ngano,manna mpya, ni kipaji ambacho Yesu alitaka kitumike siku zote kugeuza kuwa mwili wake wakati wa Misa.
 Divai- Ni kinywaji, alama ya sherehe,sasa Kristo naye anatuchangamsha na damu yake itokanayo na mazao ya binadamu yaani Divai, rejea Sala ya Mt.Inyasi
 Maji- Maji ishara ya uhai, huchanganywa na divai, maji yalitoka ubavuni pa Kristo, maji yanaonesha utakaso wa kisakramenti.Rejea sala ya Mt.Inyasi
ishara nyingine mbalimbali hasa wakati wa ibada ya misa ni:
Kupiga magoti, Kuibusu Altare, Kuinama, Kusimama au kuketi kanisani. Kukaa kimya Kwa muda, Kufukiza ubani, Kunyunyiziwa maji ya Baraka, Kuimba nyimbo, Kusoma neno la Mungu, Kupeleka maombi yetu, Kutoa sadaka na vipaji, Kuumega mkate, Kutakiana amani N.K, nitavichambua baadaye kidogo hebu tuendelee na Misa,
MISA ni upyaisho/ukumbusho wa kweli wa sadaka takatifu iliyotolewa na Kristo mwenyewe Msalabani,Ni sadaka ya sifa,shukrani,kuomba huruma na kufanya malipizi.Hapa ndipo kanisa lote la Mbinguni, Toharani na duniani (KKK namba 960) wanashiriki furaha ya milele japo wa duniani furaha yetu hiyo hatuipati kwa ukamilifu lakini kama watakatifu Mbinguni nasi tutamwona Bwana ana kwa ana siku moja tukiishi vema. “walipo wawili watatu nami……nipo katikati yao”rej.Mt.18:20, kumbe Katika Misa Mungu yupo katikati yenu kweni tumezidi hata wawili, hata akiwa kuhani peke yake bado yupo na Marehemu wa toharani nasadaka yake inasikika kwa Bwana. Misa takatifu kumbe ni Kristu mwenyewe kuendelea kujitoa kwa MUNGU na kwa Kanisa lake, tena ni Kalvari kurudi tena altareni, ni upendo mkuu kuendelea kutolewa madhabahuni/ altareni.
Katika Misa Takatifu Kristo yupo nasi kweli -i-katika nafsi ya Mhudumu/muadhimishaji(padre au askofu) - -ii-kwa njia ya Neno Lake na - -iii-katika maumbo ya Ekaristi takatifu ,REJEA KKK- Ukurasa wa 269 na SC.7. pia hata katika kila nafsi na sura ya Muumini mwenzako Kristo yupo.
Lakini pia Misa Takatifu ina sehemu kuu mbili kama liturjia; MOSI-Neno, PILI-Ekaristi,na sehemu ndogo ni Utangulizi na Hitimisho/Baraka ya mwisho., kumbe ina vipengele vinne ,vyote ni sharti tuvishiriki.
MISA takatifu huadhimishwa kwa kuongozwa na padre au askofu,na Ekaristi lazima iwepo kwani hicho kiini cha sadaka ya misa na hayo mambo ndiyo yanayo tofautisha Ibada ya kawaida na Ibada ya Misa.
Ibada ya kawaida inaweza kuendeshwa na katekista au muumini yeyote Yule anayeelewa mwongozo.Kwa kweli Misa ni fumbo kwani inahusika na mambo yasiweza kuonekana kwa macho yetu wala kushikwa na mikono yetu,tena hapa mtu asijidanganye kuing’amua Misa kiakili zaidi, uwiano wa akili, nguvu,roho na moyo ni muhimu uwepo, hapa ndipo tunamuomba Mama aliyeishuhudia Sadaka hiyo kwa macho yake atuombee kwa Mchumba wake(Roho Mt.) ili kwa Mwangaza wake tulifaidi na kulichukua rohoni fumbo Hilo KUU,
Padre akiwa anaingia Kanisani kuadhimisha Misa Takatifu , hapa unaweza kuona fumbo hili ni kama Padre anapanda ngazi kuelekea chumba cha juu cha kuila kalamu ya Bwana ambapo waamini wanaruhusiwa kumfuata huko ili kuianza sadaka takakatifu pamoja na Kristo na mitume wake alhamisi kuu Mt 26:17-30.Hivyo tutokapo Nyumbani pengine tupunguze hadithi za mipira na tamthiliya,badala yake tuanze kuongea rohoni mwetu hivi “leo (Dominika au misa yoyote) naenda kufanya nini?,ni nani namfuata huko?,hivi najazwa na taarifa kwamba Kristo ananisubiri Kanisani?,Hivi tunaingia na unyenyekevu kama ule wa Petro katika mtumbwi wake,Mtumbwi wa kanisa? Akasema “Bwana ondoka kwangu kwani mi ni mdhambi”Lk 5:8,kiukweli atakayeiga unyenyekevu kama huo wa Petro ataifurahia Misa na kumtukuza Bwana daima,
Kifupi mimi kwa hekima ‘ kiduchu’ niliyonayo vitu vichache naweza kujishauri na kuwashauri ndugu zangu ili vitusaidia katika tafakari, - kabla na wakati wa Misa tuzangatie vitu vifuatavyo-
Kwanza; UKIMYA- Mungu anapatikana katika utulivu , katika kelele hamna jipya ila kuna kurudia rudia tu,ukimya utengenezwe maeneo yote kutoka nyumbani,njiani hadi kanisani nje na ndani hadi sakristia ili akili za watu zitulie bila shaka unapomsubiri Mkubwa au mfalme ili uongee naye utamsubiri kwa nidhamu sana ukiwa umekaa sebuleni pake utatulia kwa ukimya na siyo kubwekabweka malangoni pake, sasa unamwonaje YESU?, unadhani anakuja kucheza soro au bagadu hapa?, anakuja kutoa sadaka kubwa basi umsubiri kwa utulivu na siyo kwa hadithi za akina madenge,akina yanga na simba, Chelsea ,Man U, Real Madrid au Bongo Movie,tupunguze hadithi kabla ya misa ndipo Mungu atazidi kujifunua moyoni mwako ili akujulishe ni nini anaenda kufanya altareni, Lengo la ukimya huu ni kuruhusu sauti ya Roho Mtakatifu isikike vyema katika mioyo yetu, na kuunganisha sala zetu binafsi kwa karibu zaidi na neno la Mungu, na sauti ya kanisa ,Nabii Eliya hakumuona Mungu katika upepo wenye Kelele bali katika upepo uliotulia Mungu anapatikana mazingira tulivu mazingira ya tafakari, rejea 1Fal19:12.
Pili; SADAKA- anayetoa hupewa, kutoa ni kupokea, hivyo jitahidi muda wote kabla ya Misa uwe na rekodi ya majitoleo yako ya juma zima au siku nzima, pia siku ya Misa uwe na cha kumpa Bwana kupitia Kanisa, hakuna asiye na cha kutoa, kilema wa miguu anao mdomo wa kufariji wengine, Kipofu pia, maskini wa mali anavyo vipaji vingine vingi sharti avitumie kwa Bwana, si kiasi kinacho angaliwa bali ni moyo wako umetoa kwa uaminifu na kwa ukweli bila dukuduku?, mjane alitoa kwa Eliya kwa moyo naye alipewa zaidi 1Fal 17:15-16, Yesu alimsifu mama aliyetoa kidogo machoni kumbe ni kikubwa machoni pa Mungu amemzidi hata Farisayo (B).
Tatu; SALA- Sala ni kuongea na Mungu, ni furaha iliyoje kuongea na Mkuu kuliko vyote?, sala inatia hamasa, sala inafungua moyo, roho, akili na nguvu ya ndani, sala inakufanya unakuwa mkubwa
rohoni,sala safi ni funguo ya kiroho, sala ya kutoka kichwani inayofuata matashi ya Kanisa au sala ya Kitabuni iliyoandaliwa na Mama Kanisa ni njema kabisa, nunua Chuo cha sala au Sali sala ya kutoka kichwani Roho Mtakatifu atakusikia, Mbingu itakujibu, Maria Mtakatifu atakusaidia uling’amue FUMBO HILI KUU, Mwanasayansi mmoja Ampere alimwambia Friedrick Ozanam kuwa Yeye huwa anakuwa mkubwa anaposali tu,sala inakukuza rohoni, mfano mimi Patmos F.B.Kabla ya Misa Tak. naweza kusali hivi +“ Ee BWANA naomba unisamehe dhambi zangu nisaidie niache dhambi, nistahilishe Ee Bwana ili katika Sadaka hii ya Misa nikuone Ee Bwana, nikuone wewe katika Ekaristi takatifu,nimuone Mama Maria mama yake Yesu na wangu pia, nisaidie nikutukuze Ee YESU KRISTO Mkombozi wangu, nitoe hofu zangu na wenzangu, ubariki furaha zetu njema, uwaokoe marehemu wote Toharani, uwakumbuke wote wanaoteseka kimwili na kiroho leo duniani, Ee Bwana nakuomba, Amina!+, Yesu alisali daima Yoh 17, Lk 9:28, Ningeshauri Kanisa mahalia liandae Sala zitakazosaliwa na waamini mara tu kabla ya MISA TAKATIFU
Nne; KUPITIA MASOMO- Ndugu zangu Kanisa lina hazina ya kushangaza, Shajara ndogo na kubwa zipo kwa masomo ya kila siku, sasa kila dominika au Misa yoyote uende kanisani huku ukiwa umeyapitia masomo ya dominika au siku husika na mwaka husika, hii inakupa nafasi wewe pia ya kulitafakari NENO, nunua shajara leo punguza mbege, ulanzi, kikang’ara,bia, sigara na starehe nyingine, ili ununue Shajara Mkristo,
Ndugu zangu inatupasa sana tujitahidi kwa uwezo wetu kuzifanya Misa zetu ziwe za tafakari sana, hapa kila mtu ajitahidi kushiriki misa kitulivu na kitafakuri kabisa, tena wanakwaya wanaaswa kabisa hapa kuepuka kishawishi cha kufurahisha mwili na kufanya matumbuizo kanisani badala yake wazidi kukua katika kufuata liturjia iliyojaa taamuli zaidi kwani hapa tunatafuta chakula cha roho zetu na siyo miili kwa matumbuizo, Padre anyenyekee mwenyewe pale altareni akijua kuwa Yeye ni Kristo Mwingine katika chumba cha kalamu hiyo “Altar Christus” , kumbe akiyumba Yeye Altareni basi waamini nao waweza kuyumba kwa kuwa wana udhaifu, tuiheshimu Altare haswaaa! iliyotazamana na Tabernakulo , pia na sisi waamini tutoke nyumbani tumejiandaa kwa kusali na utulivu huku tukitambua tunaenda kuungana na Kristo katika kumtolea sadaka Bwana Mungu wetu ambayeo YEYE aliona ndiyo inamridhisha kuliko sadaka yoyote ile, kwa hivo hili ni fumbo kubwa la kisadaka zaidi kuliko zile damu za kale na za kiumbe chochote……(B),.Kwa hivo tumuombe Mama aliyeshuhudia sadaka kwa macho yake Yohana 19:25-25, na ameishiriki kikamilifu wakati huo na anaendelea ili atuombee kwa Mchumba wake atuangaziaye roho zetu tuweze kulifaidi Fumbo hili la Misa Takatifu na tupate Baraka zake,
“ITE MISSA ESTE”- nenda kauishi utume, nanda kaiishi misa yaani upendo
VIPENGELE VYA MISA TAKATIFU: Hapa nitajikita zaidi katika Misa za Jumapili na sikuu kubwa ambako masomo matatu husomwa, misa za kati kati ya wiki baadhi ya vipengele/madhehebu huondolewa., Misa ina sehemiu nne naanza kizichambua kama ifuatavvyo, twende pamoja sasa,
(I) IBADA/RITI YA MWANZO; Katika madhehebu haya ya kuanzia mambo yafuatayo hufanyika kama yalivyopangwa,
 Kuhani anaingia- Tunasima kuonesha tunakubali mamlaka ya Padre anayekuja kuadhimisha Misa takatifu na kanisa lote, tukimpokea Yeye Tumempokea Aliye mtuma ambaye ni Kristo.
 Kubusu altare: Ni ishara ya heshima kwa Altare kama sehemu ya kutolea sadaka takatifu, mwanakondoo anaenda kuchinjwa hapo tena, altare ni kalvari ya karne zetu.
 Ishara ya msalaba – Padre anatuanzishia Kuukiri utatu Mt. na kujikabidhi kwa utatu, Pia msalaba ni jukumu, jukumu letu ni kuuishi upendo, Kumbe ishara hii unaweza kuitafakari na Mungu akakufundisha mengi, tuache ishara za kichoyo, tufanye ishara ya Msalaba ya kweli, Mungu Baba aendelee kutuumba wengi tumejibomoa sana, Mwana atukomboe jamani wengi bado tunakimbizwa na utumwa huku bondeni, Roho Mtakatifu atufariji, atujaze mapaji, afungue akili zetu, KWA JINA LA BABA NA LA MWANA NA LA ROHO MTAKATIFU, AMINA!
 Salamu- “Bwana awe nanyi…” hii salamu husemwa takribani mara tano ndani ya Misa, sisi hujibu “ na awe rohoni mwako” , kuhani aseme kwa upendo na hamasiko la kiasi na waamini tujibu kwa furaha na uzuri, tukumbuke Kristo ndiye anayetuambia Bwana awe nanyi na siyo Padre kwa mwenyewe, Kristo anatumia midomo ya Padre kutusalimu, nasi tumjibu Kristo kwa uzuri na hekima tafadhali. Padre anaeleza kidogo juu ya Misa ya siku husika, pia kama nia za Misa zipo huzisoma basi nasi tusisite kuziombea na kuunganisha nia zetu binafsi
 Kujuta dhambi (Penitential rite)- tunajuta tukiwa tunapiga magoti ishara ya toba na unyenyekevu labda sehemu iwe haifai kupiga magoti au una matatizo ya kiafya unaweza usipige, Tunaenda kufanya jambo takatifu ni lazima tuzidi kujiosha tu, tumetumia maji ya Baraka mlangoni tunajibariki, tena saizi tunatubu dhambi, tena tutakiri baadaye, hatuchoki kuomba msamaha kwani sisi ni wadhaifu, lakini tukumbuke toba hii si sawa na ile ya Sakramenti ya Upatanisho kwa hiyo kitubio kwa Kristo Kupitia Kasisi “Mshenga wa Kiroho” kipo pale pale, hapa tutubu toka rohoni kabisa lasivyo Kristo hatapokea sadaka yetu.
 Bwana utuhurumie (Kyrie Elei son)- tumejuta dhambi hatuchoki kusema Bwana atuhurumie, tusijifanye kama sisi ni wasafi, ole wetu Tusije tukawa kama miji isiyotubu Mt 21:20!, Mtoza ushuru ananyenyekea kuwa yeye ni mdhambi na anasamehewa LK 18:13 “Ee Mungu uniwie
radhi mimi mdhambi…”, kumbe nawe sasa wasamehe wote waliokukosea wazima na wafu, waombee msamaha kwa Mungu waliotoharani.
 Utukufu kwa Mungu juu Mbinguni (Gloria)- ungana na Malaika, Maria, watakatifu na waamini wote tumtukuze Bwana, kama malaika waliimba utukufu mara tu alipozaliwa Huyu Mwana wa amani LK 2:13-14, iweje mimi na wewe?, tuimbe wote tusiiachie kwaya tu, Ee Kristo mwana wa Maria utukuke!,Utufu hauimbwi kipindi cha maajilio na kwaresma kwani ni vipindi vya toba.
 Sala fupi ya ufunguzi- Padre anaongoza sala ya ufunguzi ambayo hutofautiana kutokana na vipindi vya liturjia ya Kanisa, yatupasa kujibu Amina kwa moyo kabisa, tuna amina takribani kumi na moja ndani ya Misa., Amina hii huhitimisha riti hii ya utangulizi.
(II) LITURJIA YA NENO; Hapa hujumuisha Somo la Kwanza, Lapili na Injili katika Misa za Dominika na sikukuu kubwa za Kanisa, lakini siku za katikati ya wiki Masomo husomwa mawili tu, Neno ndiye Kristo mwenyewe ndiye Mungu mwenyewe Yoh 1;1-, neno lina nguvu sana katika maisha yetu, maneno hutuwezesha kushirikishana furaha na machungu katika maisha yetu, dunia ingekuwaje kama maneno yasingekuwepo?, yaani tungekuwa bubu wote?, lakini Kristo anatupa neno la uzima, Mungu pia anatumia neno kuawasiliana nasi kwa lugha nzuri, hadharau lugha yetu, Kabla ya Mtaguso wa Vatikano wa pili Lugha ya Kilatini tu ilitumika duniani kote katiak Misa, lakini wafasili ni wengi na lugha zimekua ndio maana mtaguso uliruhusu Misa ziweze kufanyika kwa lugha ya mahali husika, Mfano Kilatini- Deus, Kiswahili “Mungu”, Kiarabu – Allah, Kiingereza God, Cha kuzingatia lugha itafsiriwe vema na kwa usahihi,
Kwa masomo matatu, Somo la kwanza hutoka agano la kale , somo la II hutoka katiaka Matendo ya mitume,Kitabu cha ufunuo, au nyaraka za mitume kama Paulo, Petro, Yohana, Yakobo/james na Yuda. Na somo la tatu hutoka kati ya injili hizi nne yaani Matayo, Marko, Luka Na Yohana.
Somo la kwanza; somo hili hutokea Agano la kale(AK) yaani kati ya vile vitabu 46 vya AK, muumini aliyeandaliwa husoma, ingefaa wasomaji wapitie kabla masomo haya ili kusiwe na kurudia rudia na kuwapotezea umakini washiriki wakati wa ibada, tusilipuelipue mambo ya Mungu, tusome na tusikilize kwa makini tukiyaweka moyoni kwa tafakari, acha biashara nyingine kama si za mhimu wakati masomo yanasomwa huko ni kama kumkosea Mungu.
Wimbo wa Katikati: Mara nyingi huchukuliwa kutoka kitabu cha zaburi pia manabii, sikiliza tafakari wimbo huo ambao huimbwa huku tumekaa, kama unaufahamu imba muumini usiwaachie wanakwaya peke yao, Misa ni tendo la jumla siyo la binafsi, tukitafakari wimbo huu kuna kitu Mungu anatueleza hapa.
Somo la pili; Muumini aliyechaguliwa husoma , anasema “Neno la Bwana” tunajibu “Tumshukuru Mungu”, viitikizano hivyo hufanyika pia wakati wa somo la kwanza, msomaji unavoenda kusoma somo unapaswa kupiga magoti(abudu) kuelekea Tabernakulo kabla hujapanda ngazi au kuinama kiwiliwili kama hamna Tabernakulo ila Msalaba upo, na pia ukifika mimbarini unageukia kwa Padre unainama hii ni ishara tena ya heshima kwa kuhani, ndipo basi unasoma somo kwa utulivu ila sauti isikike!, wakati wa kurudi fanya ishara zilezile tafadhali tusilipue liturjia kwa kuvipuuza vitu hivyo, vinachochea sana moyo wa ibada.
Aleluya: “hall’lu Jah- Msifuni/Mtukuzeni Mungu”, ni neno la kiebrania hilo, ni neno la shangilio, rejea Ufunuo 19:1,3,4,6, Onesha moyo wa shangilio kweli kwa kuimba kwa furaha, wanakwaya ni vema tukatafuta tyuni ambayo waamini watashiriki wote kuimba sifa za Bwana,au turudie tyuni mpya mara nyingi ili waamini wapate kuizoea na kuimba nanyi, Shairi lake hutofautiana kulingana na siku ya Misa ni ipi.
Somo la III( injili); Mwaka A-Matayo, Mwaka B-Marko, Mwaka C-Luka, Yohana inasomwa vipindi vya Noeli na Pasaka, injili ndiyo habari njema, ndiye Kristo, injili ni utimilifu wa ufunuo wa Mungu,kila Misa takatifu tunamsikia Kristo katika injili, injili hupewa heshima kubwa kuliko masomo mengine, na ndiyo maana, -husomwa na padre au shemasi,
-utangulizi wa pekee kabla kusomwa na Padre na sisi huitikia “ Utukufu kwako Ee BWANA” huku alama ya Msalaba ikichorwa kwa kidole gumba, ishara ya msalaba kwenye paji la uso,midomo na kifuani:hili hufanyika padre anapotaka kuisoma injili,hapa tunatukuza utatu mtakatifu na wokovu yaani huyo neno anayeenda kutufundisha kwa midomo ya Padre.alama hizi tatu tunazo ziweka zimekamilika kabisa kama ifuatavyo:
Paji la uso/ Usoni (+); tunamaanisha Neno likae na nilielewe kichwani/akilini mwangu,
Midomoni (+); nimkiri na nimtangaze/nimhubiri kwa watu bila kusita kwa maneno na matendo.
Kifuani (+); nilitafakari na kulihifadhi rohoni mwangu yaani niushike usafi wa moyo kwani mimi ni hekalu la huyo NENO.
-inasomwa huku waamini wote tukiwa tumesimama, isipokuwa, Jimbo la Songea kwa sababu za kiutamaduni hukaa wakati injili inasomwa na wamepewa ruhusa kutoka Roma Vatikano,
-padre anaibusu baada ya kusoma au humpelekea abusu kwa heshima askofu akiwepo.
-pia umalizaji wa usomaji wa injili ni wa pekee kwani huwa tuna jibu “ sifa kwako Ee Kristo”
Homilia- mazungumzo na watu kwani homilia ni neno la kigiriki, Kristo kupitia Kasisi anamwilisha maandiko kwa nguvu ya Roho Mtakatifu, Homilia hutolewa huku tukiwa tumekaa ishara ya utulivu, homilia inaunganisha neno na maisha yetu ya kila siku kama wakatoliki hivyo Padre anapaswa kujiandaa kiroho na kimwili kwa mahubiri sawia yanayoleta na yanayobeba maonyo, matumaini na mwongozo wa maisha Yetu, je tunasilkiliza homilia?, Kristo anataka kuniambia nini kwa midomo hii ya Mtoa homilia?, kuna kosa kubwa linafanyika na waaamini baadhi ambao huwa wanatoka nje wakati wa homilia au wengine huanza hadithi/ porojo nyingine na jirani zao baadala ya kusikiliza sisi tunapuuza homilia na ndiyo maana hatubadiliki kiroho, ole wetu tunaodharau kipengele chochote ndani ya liturjia tukidhani hakina umhumu, Kristo alitoa homilia wengine walidharau Yoh 6:52, Petro wakili wa Kristo alitoa homilia Mdo 2:14 Wengine walipuuza, na leo Kanisa linaendelea kutoa Homilia wengine wanapuuza, na wewe unafanya hivyo hivyo?, acha kupuuza ili utakatifuke ,haijalishi nani anayesimamama kuhubiri!.ili mradi Kanisa limempa Baraka zake.
Nasadiki (Credo)- kule Nicea mwaka 325AD(BK), Sala hii iliundwa, hapa unaposali unakiri Imani yako, Huu nu mhutasari wa Imani Yetu, tunamsadiki Mungu katika Utatu Mtakatifu, tunakiri kuwa Mungu ndiye aliyetuumba, tukaanguka topeni/dhambini lakini Mungu akaja kutukomboa kupitia Kristo aliyejimwilisha ndani ya Tumbo la Maria akachukua ubinadamu na akanyonya maziwa ya Maria, yaani Kristo alipata Midomo ya kuongelea, miguu ya kutembelea ili ahubiri huko na huko na mikono ya kuonyeshea mifano na kutolea sadaka, vyote midomo,miguu na mikono alichukua kutoka mwili wa Maria, “Kristo hakuwa na Baba Duniani ila Mama na hakuwa na Mama Mbinguni ila Baba”, tunaposema “Akapata mwili…………Akawa Mwanadamu” Tunainama ili kuuabudu Umwilisho/incarnation(kujifanya mwili kutoka kwenye Umungu/ kujifanya nyama) kwani hili ni fumbo na unyenyekevu wa Kristo, Alijishusha ili aje ateseke nasi na atuokoe kumbe lazima tuheshimu ,huu ni unyenyekevu mkubwa, si rahisi leo hii Mheshimiwa Raisi au Mbunge aachie madaraka yake na aache mali zote na arudi kwetu vijijini kule ili tulime naye na tunywe naye mbege,ulanzi, tule naye ugali wa mhogo si rahisi kabisa, Lakini Yesu hakuona shida kuzaliwa na bikira wa kawaida, baba mlishi mchongaji tu,Kristo hakuwa na nyumba,alikuwa na kanzu tu, hakumiliki mali kubwakubwa, hii ni ajabu ya Karne hasa leo wengi huogopa kujishusha, wanang’ang’ania madaraka, mali, sifa zisizo za msingi n.k. kumbe leo tunaaswa kujishusha , sasa jiulize, Je naamini Mungu Mmoja kajifunua katika nafsi tatu yaani Baba, Mwana na Roho Mtakatifu?, je, ni kweli nasadiki juu ya fumbo la umwilisho Yoh 1:14, Lk2:7?, je naamini Kristo alizaliwa kwa Bikira Maria kwa uwezo wa Roho Mtakatifu na siyo tendo la ndoa Lk 1:31?, Je naamini Kristo alivunja kuzimu akawafungulia marehemu na kufungua milango mitatu yaani
Mbingu/Paradiso Lk 23:43, Toharani Mt 12:32 na motoni/Jehanam? , Je naamini atakuja tena kutoa hukumu ya mwisho uf 20:11-15?, Je naamini katika Roho Mtakatifu? Mk 1:8,10 Lk 1:35, Je naamini katika Kanisa Moja, Takatifu, Katoliki na La Mitume Mdo 2?, je unaamini katika ushirika wa watakatifu yaani kwamba tupo nao hata kama kimwili wameondoka duniani?, je unasadiki juu ya ubatizo mmoja kama tiketi ya kuunganishwa na Kanisa?, kumbe inabidi tutafakari sana juu ya sala hii mhimu sana ambayo ilizima uzushi wa kidini katika historia ya Kanisa na inaendelea kuvunja porojo hizo, Nasadiki ni NDIYO YETU KWA IMANI na kwa MUNGU wetu, tunapokiri kwa moyo tunamfanya Mungu azidi kuliimarisha Kanisa lake na IMANI yetu.
Sala ya waamini (Maombi ya jumla) : “anayeomba hupewa, bisheni mtafunguliwa Mt 7:7-11” Maombi haya ya siku husika au nia ya misa hiyo husomwa na Muumini husika au Katekista au Hata padre mwenyewe ingawa ushirikishwaji wa kiliturjia kwa walei ni mhimu zaidi Mtaguso wa II wa Vatikano unashauri hilo, hivyo tusikilize vema maombi haya ili tuelewe ni nini tunaomba,tutaombeje tusichokijua?, tumuombe Mungu ayapokee pia maombi hayo na yetu binafsi, tusiwasahau wasio na waombezi , tutanue sala zetu, tuombe upendo utawale duniani kote, tazama roho toharani zinahitaji niziombee hapa,sasa tuache ubinafsi tuwaombee wote hata maadui zetu na sisi tusijisahau tujiombee pia. hapa tunakuwa tumemaliza liturjia ya Neno.
(III) LITURJIA YA EKARISTI; hii ni sehemu muhimu sana katika ibada ya misa, ni hapa ambapo tunapelekwa kiroho kwa kile kilichofanyika miaka zaidi 2000 iliyopita siku ya alhamisi kuu Lk 22;19, nanukuu “ akautwaa mkate , akashukuru, akaumega, akawapa akisema huu ndio mwili wangu….. Akaendelea akakitwa kikombe akasema hii ndiyo damu yangu…”, aliwapa mitume na mahalifa wao uwezo huo wa kugeuza mkate kuwa mwili wake na divai kuwa damu yake takatifu,Yesu kusisitiza hilo kwamba Kanisa lisije likaacha utume huo wa kula mwili na damu yake, baada ya ufufuko alikumbusha tena kwa vitendo Lk 24:30 ,kwani binadamu wakati mwingine ni moyo na vichwa ngumu!, amefufuka kweli, Mitume pia waliendelea kuumega mkate wa Bwana(Kristo) Mdo 27:35, Mdo 2:42-46, 1kor11:17, Ebr10:25 Kumbe Kanisa nalo si kichwa ngumu ndo maana haliachi kufanya tendo hili duniani na Mbinguni la kugeuza mkate kuwa mwili wa Kristo na divai kuwa damu ya Kristo kwa msaada wa Roho mtakatifu Kwani ndimo linakutana na Kristo Kweli, Bila Misa hakuna kanisa,Misa ni uhai wa kanisa, ni pumzi ya Kanisa, Kanisa la mwanzo lilikuwa na Liturjia rahisi, ilikuwa sehemu yamlo lakini liturjia imeendelea kukua siku hadi siku, kwani madhehebu mengi ndani ya ibada yameongezeka ili kuinawilisha Misa takatifu lakini Kanisa linatumia mhutasari uleule uliotoka kwa Mitume wa Yesu,sasa tuangalie vipengele vya liturjia ya Ekaristi.
( A)Matoleo na kuandaa sadaka/ dhabihu
Kutoa sadaka: “Sadaka ni kujinyima vitu vya thamani(fedha, mali, nguvu au muda) na kuvitoa vitu hivyo kwa Kanisa ili kuliwezesha liendelee na kazi yake ya kuabudu na kutoa huduma" rejea Biblia ya kiafrika Uk.2213, kumbe sadaka ni kumrudishia Mungu vipaji alivyotujalia, “Basi kwa njia yake tumtolee Mungu sadaka ya sifa ndilo tunda la midomo inayoungama jina lake", Ebr 13:15, Tutoe sadaka ndugu zangu tuache mchezo tukidhani tunamzulumu Mungu kumbe tunajikaanga wenyewe, Mbinguni kunahitaji sadaka bora zaidi kuliko zile za Zamani Ebr 9;23, je tunataka Kristo aje tena atoe sadaka hiyo au tunatoa?, Anayetoa hupewa tena mara zaidi ya alichotoa, hakuna asiye na cha kutoa awe kilema,maskini,tajiri nk lakini anacho kizuri cha kutoa, sisi tunatoa sadaka lakini hatuwezi kuizidi ile aliyotoa Kristo msalabani, Sadaka si hela tu, bali ni chochote kizuri mbele za Mungu tumpe, sadaka itoke rohoni siyo ya kujivuna ,Manabii (Mapadri) wanatuambia tunakunywa lakini hatukati kiu, tunakula lakini hatushibi ni kwa sababu hatumpi Bwana sadaka kupitia Kanisa lake rejea nabii Hagai 1:5-6, tujiulize siku nzima,wiki zima tume jitoleaje katika shughuli za Jumuiya kama usafi,ujenzi,sala n.k? hizo zote ni sadaka au ndio tunaenda Kanisani hatuna rekodi yoyote ya majitoleo yetu kwa wenzetu, ndugu zangu tupeleke sadaka kwa Bwana, wakati wa sadaka ni vema mpangilio ukawa mzuri ili kutoharibu utaratibu wa Ibada.
Vipaji hupelekwa :Kama tuliandaa kupeleka vipaji basi vyombo vya Misa kama Kalisi,Siborium,n.k Pamoja na matoleo mengine hupelekwa na waamini maalumu Kwa Padre kutokea nyuma ya Kanisa, inapendeza sana kwani hapa Padre anasimama badala ya Kristo nasi kama Jumuiya na ndiyo maana tunasimama, tunaomba Kristo apokee nafsi zetu zilizo katika Vipaji hivyo na atufyonze katika fumbo lake la Upendo, mwishowe Padre hutubariki kwa Ishara ya Msalaba sasa kumbe Kristo amepokea nafsi yangu,yanipasa nijiweke tayari kuwa naye, jiulize moyo wako umempa Yesu katika Bahasha hamna au mia tano,elfu kumi, laki n.k, kikapu chako kina nini? Matendo ya huruma, au hewa?,
Kutolea mkate: Padre anachukua Patena Yenye Mkate (Hostia kubwa) na kuinua akisema kwa sauti ndogo “Ee Bwana Mungu wa ulimwengu maana kwa wema wako tumepokea mkate huu tunaokutolea, Mkate huu ni mazao ya nchi na kazi ya mikono ya wandamu, utujalie uwe kwetu mkate wa uzima wa milele”,Kumbe Kanisa linaona kabla ya kuvigeuza ni vema kumuomba Mungu na kumpa ili avibadilishe.
Kuchanganya maji na Divai : Padre anachanganya maji akisali “Kwa fumbo la maji haya na divai hii tujaliwe kushiriki umungu wa Kristo, aliyekubali kushiriki ubinadamu wetu” Kristo anasema “Mimi ni mzabibu” Yoh 15:1, kumbe divai ni Alama ya Kristo, tuanaambiwa pia “Mtu asipozaliwa upya katika maji na roho hawezi kuingia ufalme wa Mbinguni” (B), kumbe maji ni ishara ya ukombozi lakini pia maji ni alama ya Ubinadamu wetu, kumbe basi kitendo cha Padri kuweka maji(Ubinadamu) katika divai
(Kristo) ni kwamba ubinadamu wetu dhaifu huu uchukuliwe na Kristo, na ndiyo maana Maji hayaonekani tena yakichanganywa na divai ndo kusema tumefyonzwa na Kristo Yesu , ni raha ilioje kufyonzwa na Kristo?, Kristo anataka kuuponya ubinadamu wetu huu uliochubuliwa na dhambi,sisi ni matawi yake, Yeye ni mzabibu,ili tuzae matunda bora ni lazima tujishikize kwake.
Kutolea Divai : Akisha kuchanganya padre anayesoma Misa huchukua kalisi anainua na kusali kwa sauti ya chini “Utukuzwe Ee Bwana Mungu wa ulimwengu, maana kwa wema wako tumepokea divai hii tunayokutolea, Divai hii ni tunda la Mzabibu na kazi ya Mikono ya wanadamu, utujalie iwe kwetu kinywaji cha Roho”
Sala fupi -Ee Bwana utupokee sisi tunaokunyenyekea……
Kubariki na kuvufiza kwa ubani: Ubani ni ishara ya sala na sadaka kwa Mungu Zab 141:2, ubani unatengeneza mazingira ya ibada yanayoamsha tabaka linapojaa moshi mzuri wa kunukia unaamsha shime Yetu ya kiibada, Padre hubariki ubani, kishapo huvukiza ubani kuzunguka altare yote, Vipaji,Msalaba, pia kama ipo mishumaa, au pango la Mtoto Yesu n.k, baadaye Padre anafukizwa Yeye na waamini nao wanafukizwa, ni ishara pia kwamba sisi,padre na vipaji tunaenda kujitoa sadaka ya upendo na ndiomaana tunasimama kwa heshima,kumbe sisi ni wanakondoo wengine, si lazima kila MISA ubani utumike, sababu za kiuchumi na mazingira zaweza kufanya ubani usitumike, bado Misa inabaki kuwa na thamani,
Kuosha mikono: Maji ni alama ya utakaso,Padre hunyunyiziwa maji mikononi akinawa huku akisali kwa sauti ya chini “Ee Bwana unioshe kabisa na uovu wangu unitakase dhambi zangu”, kumbe Padre ananawa si kwa sababu amechafuka na vumbi au jasho bali anajisafisha kiroho tayari kwa kutolea dhabihu Takatifu., hayo yote tangu kutolea Mkate mpaka kuosha mikono hufanyika huku wanakwaya wanaendelea kuimba.
Salini ndugu: ili sadaka yangu na Yenu…….. tunajibu, “Bwana apokee sadaka mikonono mwako(padre) kwa sifa na utukufu wa jina lake(Mungu) na pia kwa manufaa yetu sisi (waamini wote) na mafaa ya Kanisa lake lote takatifu”, Misa ni kifungo cha upendo na umoja hivyo Padre akiwa amebeba nafsi zetu anatualika tuombe naye, hivyo tusisite kumuomba Bwana apokee sadaka,majaitoleo na mioyo yetu ili tubadilishwe naye.
Sala ya kuombea dhabihu; Pd…….daima na milele, tunaitikia Amina , amina hii inafunga sehemu ya matoleo.
(B) Sala ya Ekaristi
Utangulizi; Padre- Bwana awe nawe nanyi, tunajibu – na awe rohoni mwako
Padre- inueni mioyo, tunajibu – tumeinua kwa Bwana
Padre- Tumshukuru Bwana Mungu wetu, tunajibu – ni vem na haki
Padre anaendelea na utangulizi “ kweli ni vema na haki….., hapa maneno hubadilika kutokana na kipindi,
Mtakatifu (sanctus)- huu ni wimbo ambao huimbwa au kutamkwa mara baada ya utangulizi wa sala ya ekaristi, “Mtakatifu Mtakatifu Mtakatifu Bwana Mungu wa Ulimwengu, Dunia zimejaa utukufu wake” Isaya 6:3 tunaimba kinabii na kimalaika hapa, tena tunaungana na mabinti Sayuni tukisema “Mbarikiwa ajaye kwa jina la Bwana hosanna juu Mbinguni” Mt 21:9, Neno Mtakatifu tunawiwa kuliirudia mara tatu kusisitiza kuwa Yeye ni mtakatifu kweli, Hosanna ni neno la kiebrania linalomaanisha “tafadhali okoa sasa!” Mt 2: 9,15, si wale tu wana wa uyahudi bali leo tunamuomaba yeye aokoe sasa!, tena tunajua anaenda kuvunjwa msalabani/ altareni ( mageuzo ya makate na divai) ili atuokoe, sasa tuungane naye kwa shangwe na Imani tukisita kuimba sanctus hii hata mawe na miti vitasifu! Imba ndugu mtakatifu huimbwa sikuzote kwani huufahamu?, na ndomaana hata Kengele hugongwa ikiwepo ili kuonesha shangwe na shime kuwa Mwana wa Daudi aliyemtakatifu anakuja kutuokoa.
Mageuzo (Consecration)
Pd : Ee Mungu tunakuomba uibariki sadaka hii ikupendeze, uipokee ili iwe kwetu mwili na damu ya mwanao Yesu Kristo , Kengele inaweza kupigwa kwa namna husika ili kuwataarifu na kuwamakinisha waamini waelekezee macho katika mageuzo!
Baadaye Padre Anachukua Patena Na kuiinua kidogo akisema “huu ndio mwili wangu …….” Kisha anaweka juu ya korporale Na anasujudu Kwa kupiga goti (genuflection)
Kisha anachukua Ciborium/ kikombe cha divai na kuinua akisema “hiki ni kikombe cha damu yangu….”, kengele pia hugongwa kama ipo ili kutaarifu, haya ni maneno mazito ya mageuzo na yamebadilisha mkate kuwa mwili na divai kuwa damu, patena na ciborium vinaponyanyuliwa na sisi tujiweke humo tusulibishwe na Kristo mwenyewe, hapo Kristo anakufa na ndiyo maana mkate umegeuzwa peke yake na divai imeugeuzwa peke yake kumaanisha kifo,
Fumbo la Imani: Kweli hili ni fumbo/mystery (jambo lisiloweza kueleweka kwa milango yetu ya fahamu) ila katika roho tunalionja, tulipokee kama lilivvyo na tulikiri tukisema Tunatangaza kifo chake,
tunatukuza ufufuko wake mpaka atakapokuja siku ya kiyama ujio wa pili, Kristo ni mwenye upendo na unyenyekevu kupitiliza,YEYE ni Mungu,alikubali kuchukua ubinadamu tumboni mwa Maria akazaliwa , akaishi na mwanadamu, akafa kwa aibu, na bado anajiacha altareni katika maumbo ya mkate wa ngano na divai ya mzabibu mazao ya biandamu hili kweli ni FUMBO KUU tuliabudu, tulitangaze, jisemee moyoni “ole wangu mimi nisipokutangaza WEWE mwanakondoo!”
Kuliombea Kanisa, sisi,marehemu na kujiunga na Watakatifu- Huu ni wito wetu kuombeana kwa Mungu kupitia Mama Maria, Mt.Yosefu, Malaika na watakatifu wote tunawakabidhi hata viongozi wetu wa Kanisa mikononi mwa Mbingu ili wasichoke kuyalinda Matakatifu hasa Baba Mtakatifu Askofu wa Roma, wakili wa Kristo, Halifa wa Petro mtume,ishara ya umoja wa Kanisa la Duniani.
Kwa nji a yake pamoja naye na ndani yake…., Hapa tushirikiane na Padre anayetolea damu na mwili huku akiwa ameinua akisema maneno hayo, wote tunajibu Amina tuijibu kwa Nguvu, hii ni kama amina kuu,kwani Pamoja naye KRISTO, kwa njia yake KRISTO, na ndani yake KRISTO , MUNGU BABA atukuzwe katika ushirika wa ROHO MTAKATIFU, Amina hii wengine huimba mara nyingi , hapa tunapoitamka kwa dhati Amina hii tunamtukuza BABA kupitia MWANA katika ROHO MATAKATIFU.
(C) Sehemu ya Ibada ya Komunyo
Sala ya Bwana: Baba Yetu\, hapa haturudi nyuma kwenye mageuzo bali tunapiga makasia kuelekea mlo mtakatifu, Komunio takatifu, Muungano binafsi na Kristo Mungu, Hivyo tunasali sala hii kuu si kwa sababu tu tumefundishwa na Yesu la hasha! Bali pia tunaonesha kukiri udogo na utegemezi wetu kwa Bwana Mkubwa sisi ni funza tu mbele za Bwana Isaya 41:13,
Pd anasema…..Unaye ishi na kutawala daima na milele…tunajibu Amina.
Kutakiana Amani:Pd anasema ”Amani ya Bwana iwe daima nanyi” Yoh 20:19,20 Shalom! Hivi punde Tunataka kumpokea Kristo wa Ekaristi ni sharti tupatane na jamaa zetu kwanza Mt 5:23-24, Salimianeni kwa busu la upendo 1Pet 5:14, wakristo wa mwanzo walikumbatiana na kubusiana katika ibada hivyo tushikane mikono kwa tabasamu la dhati ili tuwe wamoja, ni raha ilioje Patmos anashikana mkono na Monika au Peter, Thomas na Maria, au Anna na Nguki H Engeneeer, sipati picha, inachangamsha zaidi ya chachandu!, inatuweka sawa ili tumpokee Kristo kwa uso mlaini na siyo uso wa ndimu au mkangafu,msalimie hata unayejua ni adui pengine ndiyo siku ambayo Mungu anataka mpatane, usijali si lazima umfahamu unayemsalimia, jua tu mmeunganishwa na Kristo hivyo ni ndugu mtakie Amani.
Mwanakondoo wa Mungu (Agnus Dei) NA Kumega Mkate: Deus-Mungu, Agnus-Mwanakondoo, ni walatini wanatuambia hivyo, wakati wimbo wa Mwanakondoo unaimbwa au kutamkwa Padre anamega kipande kidogo kutoka hostia kubwa kwenye Patena na kutumbukiza kipande hicho cha mwili wa Kristo katika Kalisi yenye damu ya Kristo, Kumega Hostia ni ishara ya Kifo cha Kristo, Kristo alimegwa kalvarini na leo pia anaendelea kumegwa altareni kuiendeleza kazi ya wokovu,daima Kristo yupo msalabani hadi mwisho wa Dunia kupitia Kanisa lake na ndiyo maana anamwambia “Sauli, Sauli mbona unanitesa?” Mdo 9:4 ,sasa iweje Yesu ambaye alishakufa, akafufuka na akapaa Mbinguni tena amlalamikie Paulo baadaye kabisa?, kumbe ndo kusema Kristo anaendelea Kufa na Kufufuka altareni/kalvarini kwa njia ya Kanisa lake na anaendelea kuokoa maelfu ya watu, pia kutia kipande katika damu ya Kristo ni ishara ya Ufufuko,yaani mwili unairudia roho(damu) yake, Huyu ni mwanakondoo zaidi ya ndama na chochete kilichotolewa hapo kale, basi tunaimani thabiti kabisa ya Kumwambia kwa unyenyekevu tukiwa tumepiga magoti na kusema Utuhurumie, Utuhurumie, Utujalie Amani, Ee Maria pole kwa upanga uliotoboa moyo wako, dhambi zetu zimekuumiza wewe na Mwanao mpendwa, tunaomba Amani itawale Ee Kristo.
Tazameni Huyu ndiye Mwanakondoo wa Mungu: Padre huelekea waamini na kutuonesha Hostia akiyasema maneno hayo,
Tunajibu: “Ee Bwana sistahili uingie kwangu lakini sema neno tu na Roho yangu itapona” LK 7:7, Mt 8:8, sisi tunatumia maneno hayo ya Jemedari wa Kirumi anayeonesha Imani na Unyenyekevu, inaonekana Maaskari pia wanaimani nauadilfu kwa Mungu Mt 27:54 “Hakika huyu alikuwa mwana wa Mungu”, hiyo ni changamoto kwa maaskari na wakatoliki tusio na Imani na unyenyekevu, Basi maaskari tuijongee Misa ili ubakaji, uporaji,ulevi na ugaidi uishe!, tujawe na unyenyekevu huo wa Jemedari ili tukimpokea Kristo wa Ekaristi atuhuishe kweli.
Kupokea Komunyo Takatifu: Padre hula mwili na kuinywa damu kabla ya kukomnisha wengine, ni vema Ukasali pia kabla ya kwenda kupokea, wengine husali sala ya pamoja iitwayo Tamaa “Ee Yesu Mkate wa Mbingu nakutamani, uje kwangu uliye heri na uzima wangu, uje chakula cha roho yangu unitie Imara, uje Ee Mwanakondoo wa Mungu uondoe dhambi zangu, Uje Ee Mganga wa roho uuponye udhaifu wangu, Uje Ee Yesu uungane nam, amina”, Unaweza kupokea mkononi (mkono wa kulia unakaa juu ya kiganja cha kushoto) pia unaweza kupokea Mdomoni,lakini ni vema tukawa na utaratibu mmoja jumuiya husika ili kuleta umoja, Padre/Mkomunishaji anatuambia Mwili wa Kristo tunajibu Amina inayosikikana,usihofu kupokea Yesu katika Mwili tu, eti mbona damu hamna!, la hasha!, Kristo yumo katika kila umbo la Ekaristi na katika kila chembe na tone, hivyo Yeye ni Mungu na hawezi kufungwa na udogo au ukubwa wa Hostia, wala hayupo nusunusu katika hostia na divai bali yumo mzima mzima katika Hostia vilevile
katika Damu yake, hivyo tuwe na Imani tu, tupokeapo Ekaristi takatifu nna kuishinvema tunajihakikishia maisha ya milele Yoh 6:58, Tupokeapo Ekaristi takatifu tunakuwa akina Maria wengine yaani matabernakulo wengine kwani tumepokea kilicho safi baada ya kupashwa habari na Roho wake, Ekaristi kama Hostia ni Manna mpya Kut 16:4 kwani wao walikufa sisi hatutakufa kama tukiila vema, Hii pia ni zaidi ya damu kondoo wa kale Kut 12:13 ni mpya huyu Ebr 9:12, Kanisa linatutaka tusile cakula saa moja kabla na baada ya Kupokea au kwa urahisi saa moja kabla na baada ya Misa,hapa tunaepusha kumkufuru Yesu wa Ekaristi tusije tukamchanganya na sembe, mbege,mnazi au mbitu,lakini kwa anayesafiri umbali mrefu au mgonjwa anaweza kula au kunywa dawa kwa maji, ukishapokea na kula hakikisha unamshukuru Mungu pia waweza kutumia sala ya Mt.Inyasi wa Loyola.
Sala Baada ya Kumunyo:Tuombe…..
Matangazo: Katika Misa Takatifu taifa la Mungu linakusanyika,Ratiba, Barua na matangazo mbalimbali kama ya watakatifu, ndoa na mikutano ya jumuiya, hapa walei wakiongozwa na Katibu wamahali husika hushiriki kila mmoja kwa fursa yake, jiulize unashirikiana na wenzako?, je unashirikisha vipaji vyako kwa Mama Kanisa?, jiulize sasa, wengine huwa wanatoka wakati wa Matangazo hilo ni kosa kwani Baraka ya Mwisho Hajatoa , mwishowe Padre huhitimisha matangazo kwa kutangaza yale yake kwa ajili ya Kanisa, Basi ni vema matangazo yapangwe vema.
(IV) RITI/IBADA KUMALIZIA/HITIMISHO; Bila kumaliza na kipengele hiki basi hujamaliza Misa, kumbe huruhusiwi utoka mpaka ukamilishe sehemu hii ya Misa.
Baraka za mwisho:
Padre: Bwana awe nanyi, tunajibu awe rohoni mwako, Tunainamisha vichwa kidogo huku tukiomba Baraka zake Mungu, Padre anatupa Baraka kwa kuifanya Ishara ya Msalaba kutuelekea waamini, basi nasi huku tukiwa tumeinamisha vichwa tunafanyaishara ya msalaba tukiwa tumekusanya maombi yetukwaajili ya Kanisa na Imani yetu, tunajibu Amina ili Mungu atufanye mitume tukampeleke Kristo ulimwenguni kwa maneno na maisha yetu ya Upendo, Padre anatuambia “nendeni na Amani”, Tunajibu tumshukuru Mungu,kwa maneno mengine tunaambiwa hivi “ITE MISSA EST” –nenda kaiishi misa(upendo) huo ndo utume tunaopewa na Kristo na Kanisa,
Kutoka nje: Waamini wote wakati padre anatoka altareni tunasimama kuonesha utii wetu kwa mamlaka ya kikuhani ,padre hubusu tena altareni kama mwanzo alama ya heshima kwa sehemu hiyo ya sadaka takatifu,wimbo wa mwisho huimbwa kwa kuongozwa na kwaya,tusimama au kupiga magoti pia mpaka Padre na watumishi wanaingia sakristia , Watumikizi hutangulia na Padre hufuata nyuma, Kama askofu yupo basi atakuwa wa mwisho katika mlolongo huo wa kuelekea sakristia au nje.
Waamini nao humalizia kwa sala fupi mathalani kwa sala ya +Nakukimbilia mzazi mtakatifu wa Mungu……., Moyo Mt.wa Yesu ,utuhurumie, Bikira Maria Mama wa Mungu ,utuhurumie, Mt.msimamizi wa Parokia/Jumuiya ,Utuhurumie, Mt.Yosefu,Malaika na Watakatifu wote wa Mungu, Mtuombee+, Tunataja kutokana na daraja, La kwanza Mungu (Yesu)- Latria(Kuabudu), La Pili Bikira Maria – Hyperduria (Heshima zaidi ya watakatifu), Latatu ni Malaika na watakatifu- Dulia(Heshima ya watakatifu), Kabla ya kutoka yatupasa tupate dakika chache ikili tuafakari sadaka kuu tuliyoifanya na Kristo leo,na kumuomba tena Mungu , Tafadhali siyo mara tu unakurupuka kwenda nje na unasahau hata ulichofaidi wakati wa Misa huoni kama unamkosea haki Yesu wa Ekaristi, chukua hata dakika moja piga ngoti yaweke matunda yote ya Misa moyoni yapange vizuri,usiwe na haraka, mambo mazuri hayahitaji kulipuka au papala ni taratibu tu Iruhusu Misa iliyopita nipenye kona zote na Moyo ndipo utoke!.
ALAMA NA ISHARA NA MATENDO MBALIMBALI NDANI YA MISA TAKATIFU
Yamelezewa tena zaidi kama ifuatavyo,
(1)MAJI YA BARAKA:Ni ukumbusho waFumbo la Pasaka na ubatizo pia kwamba kwa ubatizo tulipewa uzima wa milele,,kwa hiyo padre anapotunyunyizia maji labda katika vipaji hapa hutubariki na kutukumbusha ubatizo wetu,kwa hiyo Maji haya ni kisakramenti pia. Maji hubarikiwa kwanza na Kasisi kwa kutumia dhehebu/fomyula za kiliturjia huchanganya pia maji kuakizi tendo la Mungu kupitia nabii Elisha 2Waf 2:20-22, Basi kumbe hata katika misiba maji hutumika kukumba kuwa lipo tumaini la ufufuko wa mwili pia hilo ndilo fumbo la Pasaka,Marehemu anapigwa mhuri wa maisha ya milele tuthamini sana Ibada za mazishi, Na tuingiapo kanisani huchovya maji ya Baraka Kama kujitakasa Na kujiweka tayari Kwa Ibada, hapa hakuna sala maalumu ingawa wengine hutumia sala kama hii “Sasa naingia mahali patakatifu, Ee Yesu nisaidie kukaa kwa heshima na ibada ndani ya Nyumba yako takatifu”, pia tutokapo hatuchoki kujikumbusha ubatizo wetu na kupata tumaini zadi la ufufuko(pasaka), Hivyo penye uwezekano maji ya baraka yawekwe nyuma ya milango ya Kanisa kama viriba vya milangoni vipo.
(2)KUPIGA GOTI LA KULIA NA KUINAMA:haya ni matendo ya kuheshimu na kuabudu ikitegemea tendo anafanyiwa nani na kwa nia ipi.Tuingiapo na tutokapo kanisani huinama au kupiga goti la kulia mbele ya Msalaba au Tabernakulo,Hapa tunamuabudu Kristo aliye msalabani na anayetusubiri katika Hekalu lake(Tabernakulo),pia hakuna sala za jumla katika matendo haya lakini muumini tafakari kwa kina sana juu ya Huyo mwanakondoo aliyemo ndani ya Tabernakulo na umwambie chochote akusidie, kwa msaada sala zifuatazo zaweza kukusaidia
-Goti la kulia kwa tabernakulo,Sala-”tusifu na kuheshimu siku zote Sakramenti Kuu” au
“Ee Yesu wa Ekaristi nakuabudu”
-kuinama Kuelekea Msalaba uingiapo:Sala-”Ee Yesu nakuabudu nakushukuru kwa kuwa umetukomboa watu kwa msalaba wako Mtakatifu”
-Na pia katika Nasadiki “…akapata mwili… kwake ye Bikira Maria,akawa mwanadamu…”,Hapa fumbo la UMWILISHO linaabudiwa rohoni mwetu kama mamajusi wanaoenda Bethlehem na kumsujudu Mtoto ambaye hajaung’ang’ania Umungu wake na kuamua kuja mwenyewe katika maisha ya chini kabisa kupitia Mwanamke Bikira,kitendo hiki cha Mungu kujishusha na kujimwilisha hakina budi kuabudiwa,kwani bila hicho mwanakondoo aliyechinjwa msalabani ili tukombolewe asingekuwepo,
kumbe hapa kila mtu ainame tene mwinamo wa mwili/kiwiliwili na siyo kichwa tu, pia katika sikuu za Bikira Maria KUPASHWA habari na sikukuu ya KRISMASI wote hupiga magoti kwa heshima ya pekee ya kuabudu fumbo hili la Yesu kutwaa Mwili.
(3)MAANDALIZI BINAFSI:Aliyefika kanisani kwa kuwahi hukaa au hupiga magoti na kusali sala za kutubu kushukuru na kumuomba Mungu amuongoze kiibada,maeneo mengine waumini husali sala za pamoja zaweza kuwa za asubuhi basi katika hili jumuiya na makanisa mahalia yafanye kitu kuwandaa watu kiibada na kila mtu binafsi achukulie uzito wasaa huu kwa kuitafakari misa inayofuata punde na nia zake zote na atulie.
(4)KUSIMAMA:Hili tendo tunalianza mwanzo mwa misa wakati Padre/Askofu,Shemasi na watumishi wanatoka Sakrastia au nje kwa maandamano kuelekea altare na pia wakati anatoka kanisani,Hapa tunakubali mamlaka zao(Padre,Askofu n.k) na tunatoa heshima kwa mioyo minyenyekevu kwa mamlaka ya hao waadhimishaji wa misa ikisindikizwa na zaburi kwa furaha ya ndani kabisa,kama waumini tunaoungana na Padre anayeelekea kwenye chumba cha kuila kalamu ya pasaka alhamisi kuu pamoja na
Kristo na mitume,na hapa si Padre kwa Yeye anayetuita ni YULE Aliyeko kwenye chumba hicho cha Kalamu ya Bwana. Hapa Mwanakondoo anaenda kutulisha neno na Ekaristi katika hivyo viwili ni Yeye Mwenyewe.
-Kiufupi hii ni ishara ya heshima na kuyakubali mamlaka ya huyo muadhimishaji wa misa(askofu/padre n.k).
(5)KENGELE:Mara nyingi hii hugongwa wakati wa Padre/Askofu,Shemasi,na watumishi waingiapo(Siyo lazima), pia kwenye wimbo wa “ Mtakatifu Mtakatifu Mtakatifu” Sancti Sancti Sancti na katika kipindi cha mageuzo,
Kengele mara nyingi ni tendo la taarifa na ishara ya Shangwe au Kushangilia pia inaamusha mazingira ya sala,
-Wimbo wa Mtakatifu: hapa kengele huonyesha shangilio kama Nabii Isaya alivyowaona Malaika,Isaya 6:3,hapa tunamshangilia Mtakatifu wa Watakatifu na kumsifu YEYE.
-Katika mageuzo: Kengele hapa inawaarifu waamini mageuzi yapo hatua ipi na kuongeza umakini wa kiroho katika tafakari ya kuling’amua fumbo hilo KUU kabisa,kwani kabla ya mtaguso wa Vaticano II shida ilijitokeza ambapo baadhi ya waamini walikosa umakini kwa kufanya mengine badala ya kukazia macho ya roho zao kwa hilo Fumbo la Mwanakondoo kuendelea kujitoa mpaka leo Altare ya duniani na mbinguni.
(6)UBANI: ni aina ya dutu ambazo hutokana na ute na kuchomwa wakati wa ibada na hutoa harufu,Ubani upo kutakatifuza,kuvijali vitu vitakatifu na ni ishara ya sadaka na uwepo wa Mungu na ni tendo la kiroho tangu ibada za waisraeli Zab 141;2, hapo kale mpaka leo kanisa linapokea kitendo hicho ndani ya liturjia yake na tujue Misa ya Mbinguni ubani unatumika pia rejea Ufunuo 8:3-4,5:8…,Askofu au Padre huvukiza ubani kuzunguka Altare,Msalaba na Mimbarini wakati wa kusoma injili,pia padre mwenyewe huvukizwa ubani na mtumishi au shemasi,pia wakati wa mageuzo Ekaristi huvukiziwa ubani na mtumishi akiwa amepiga magoti,na waamini wote huvukiziwa ubani,Kati ya vitu vitatu alivyozawadiwa Mtoto Yesu ubani ulikuwepo Mt 2:11, Ubani unatengeneza mazingira ya kiibada ni ishara ya sala ipaayo kwa Mungu Uf 8:3-5
Hapa padre na waamini wanabarikiwa, kutakaswa na kujiandaa kujitoa sadaka kwa kila mmoja kwa mwenzake pamoja na Mwanakondoo Mkuu Mbele ya BABA WA MBINGU,Ubani tazama Zaburi 141,Malaki 1:11,Lawi 23:18, Kut 30:1-10,Hesabu 7:13-17, Mt 2:11, Lk 1:8-12,
HITIMISHO
Mwisho namshukuru Mungu, najua ni Yeye anayenipa nguvu na kunishughulisha na mambo haya ya Liturjia, nawashukuru wote walionisaidia hapa na pale, kidole kimoja mbele ya Chawa ni Mbwembwe tu, basi najua mliniongezea vidole na ndio maana nimefanikisha kuchapa kazi hii, kosa lolote ndani ya kazi hii nichapwe Mimi na mwenzangu, msisite kuturekebisha,daima tukumbuke kuombeana, naombeni nifunge domo langu kwani huwa linapenda kuongea sana likipewa nafasi, nikomee hapa ndugu zangu, Kwa Maombezi Ya Mama Maria mshiriki wa MISA tangu utoto wa Yesu mpaka Golgotha na hata leo atuombee ili Upendo wa Mungu uwe nasi sikuzote, Amina!
Hili nit oleo la Pili
Tolea la kwanza:
Liliandaliwa na kaka Frument Nelson (Animal Science mwaka tatu-2013)
Patmos F.B.(Agronomy Mwaka wa kwanza-2013),
na hili nitoleo la pili lililoandaliwa na Patmos F.B( Mwaka wa pili Bsc.Agronomia-2014)
+TUMSIFU YESU KRISTO+
FLUMENT, NELSON MJUNI (BSc. ANIMAL SCIENCE-SUA 2010-13. >0784-770599/ 0752-767485
PATMOS FRANCISCA BONIFAS -BSc. AGRONOMY –SUA 2012-15<> 0753412987/ 0654412987
ORODHA YA REJEA
I-Sr.Charlene Altemose MSC/What should you know about the Holy Mass/St.Pauls-Mumbai-2009
I1- Divine office 180-224
III- Katekisimu ya Kanisa Katoliki (KKK) Kubwa
IV-Sacrosactum concillium-ni hati juu ya liturjia katika mtaguso wa 2 wa Vatikano (1962-65)
V- Titus Amigu (Padre)-Kisa cha imani, Peramiho-uk-93, 2003.
VI- Titus Amigu (Padre)-Maswali wanayobandikwa Wakatoliki, Imprimatur Na Polycarp Cardinal Pengo Peramiho2008 pg 196-205,
VI-Corma Burke/Articles the Mass explained/ Monica; sinag-Tala publisher, 1981, imprimatur by Joseph T.O’Keef-Vica General Archdiocese of Newyork
VII- Ven.Archbish.Fulton J. Sheen THE HOLY MASS-You tube.
VIII- IBADA NA SALA/ BARAZA LA MAASKOFU TAZANIA ( TEC)/2013
IX-Druck: J.Kral /HOLY MASS/Kimehaririwa na Mheshimiwa.Father F. R./Abensberg/1994
X-Biblia ya Kiafrika/Mhariri Mkuu Pd.Titus Amigu/Imprimatur na Ask.Yuda Thadeus Ruwa’ichi/Paulines publication/2010.
XI- UTARATIBU MKUU WA MISALE YA KIROMA, Baraza la Maaskofu Takatifu Tanzania (TEC)-2002
Comments